Friday, April 1, 2011

Nani kama mama-26



‘Mwanangu safari yangu ya kwenda kutibiwa India ilinijia kwenye ndoto,  siku ile nilipokuwa nimezirai sijitambui, na kila hatua ilijionyesha wazi ndani ya ndoto, na kama ningekuwa najua kuwa ni kweli ningeliwaambia kuwa msiwe na wasiwasi, lakini sikuwa na uhakika nini tafsiri ya ile ndoto, kwani nilikuwa nusu mfu. Niligundua ukweli wa ile ndoto nilipokuwa nasubiri urekebishwaji wa sura yangu.
Nawashukuru sana wafadhili waliojitolea kuhakikisha narudia hali yangu ya awali, kwani sikuamini pale nilipoambiwa nijitizame kwenye kiyoo, ilikuwa kama najiona wakati nipo msichana…’ aliongea mama huku namtizama bila kuamini kuwa yule mama aliyekuwa na sura ambayo wengi waliamua hata kumuita mwanga kwa ajili ya michirizi na kuchanikachanika usoni, na sura kuwa ya kutisha, leo hii ni mwanamama mwenye sura ya kipekee…Mama mrembo na hayo macho…akajikuta akitabasamu akisema moyoni, ama kweli mama alijaliwa uzuri
‘Mungu ni mkubwa mama, siamini hadi sasa naona kama namtizama ndugu  yako, kwani sikumbuki kuiona sura yako ukiwa katika hali nzuri kama hii, mpaka uliponionyesha picha zako kabla ya kufanyiwa upasuaji na baada…kweli tuwashukuru sana wataalamu, tuwashukuru sana madakitari ambao fani yao  kwakweli ni ya kujali uhai wa mwanadamu…’ nikasema huku machozi yananilenga lenga
Mama akaongezea kusema, `Kumbuka nilikimbiwa, niliitwa mchawi, nikadharauliwa sababu ya  sura ile, ambayo sikupenda kabisa iwe vile, ila ni kwasababu ya watu wenye roho mbaya, na sijui baba yako huyo yupo hai au walimuua, maana kijijini kule kuuana ni kama jadi, na sijui yuke mwanamke wake atakuwa wapi, siku nikikutana naye …kutachimbika…’ mama akasema huku machozi yanamtoka, nami nikainua mkono na kumfuta yale machozi.
‘Mwanangu ndani ya ndoto yangu niliota kuwa upo katika hali mbaya, na  yale yaliyomfanya mama yako akimbiwe kuwa ni mchawi, yamekuandama kwa namna nyingine, watu wamekuwa wakikumbia eti  kwa vile wamekuona umekonda, wanahisi umeathirika….yote hayo  niliyaona kwenye ndoto kwa namna ya fumbo, lakini usijali mwanangu kwani yote hayo ni mitihani ya kimaisha, ikija unatakiwa uwe na subira, na usimamie katika haki…’ mama akanishika kichwa.
‘Mama unakumbuka uliwahi kunihadithia maisha yako ulipopitia na  nakumbuka ulikatisha siku ile ulipozidiwa ukashindwa kunimalizia kuwa ilikuwaje , je yule mama kule hospitalini alikuwa wewe  au nani na siku ile alipoondoka kule nyumbani kwa dada yake nesi alikwenda wapi na je alimpataje mtoto wake, na huyo mtoto ndio mimi au alikuwa mwingine…?’ nikamuuliza mawali mengi kwa pamoja.
Mama alimwangalia mwanae kwa muda, halafu akatabasamu na kusema, ‘hivi mwanangu bado una hamu na vidonda vinavyoonza kupona, huoni ukiyawaza hayo , ukayahadithia , yanatia simanzi , na mwishowe unakaribisha hasira za visasi, mimi naona  tusahau hayo tuganage yajayo…’Mama akasema akiinuka kuondoka
‘Mama ni vyema nikajua wapi nilipotokeaa ili niweze kujilinda, kwani nitasema mimi nilitokea wapi na kwa mafano baba akija leo kundai kuwa ni mwane nitamwambiaje…au…mama naomba unimalizie kile kisa kama hutojali..’ nikamsisitizia mama. Na mama akaniangalia tena , halafu akaanza kunihadithia pale tulipoishia.
‘Mwanangu, siku ile nesi na dada yake walijikuta wakifurahia ujauzito  ambao kwao ulikwa kama mgumba kupata mtoto, kiasi kwamba walijisahau nini kilichokuwa kimewaleta pale, na docta bosi wake alipoona vile akapendekeza nesi abakie pale siku ile hadi Jumatatu, kwani ilikuwa siku ya Ijumaa, na wao warudi mjini kama wataonana na yule mwanamke watamshauri afanye subira ili taratibu zifanyike za vipimo na mambo mengine, na kama mtoto ni wake atakabadhiwa. Wakakubaliana hivyo…na wao wakaondoka huku nyuma wakamuacha nesi akifurahia na ndugu zake.
Docta wao wakarudi mjini hospitalini, na walipofika hospitali wakakuta taarifa kuwa yule mama alifika, lakini safari hii alikuwa mpole na mstaarabu sana, akauliza mtoto wake yupo wapi, alipoaambiwa kuwa nyie mumeondoka kuja huko kijijini, akainuka kwa hasira na kusema,
‘Hivi mnafikiri kama ingekuwa nyie, mngefurahia hili mnalonifanyia, hivi kweli mnapenda mama atengane na mtoto wake hivihivi…sikubali, nitampata mtoto wangu mpende msipende…subirini…’ akaondoka, na haijulikani kuwa alielekea wapi.
 Docta na wenzake  walidhania kuwa huenda karudi huko kijijini na kwa vile walishaweka mambo sawa, haitakuwa na maneno, akifika huko ataelekezwa la kufanya. Siku ya Jumamosi kukawa na mawasiliano kati ya docta bosi wa nesi kumuulizia nini kinaendelea huko kijijini na kujua kama huyo mwanamke keshafika huko au bado! Cha kushangaza taarifa zilizofika ni kuwa yule mama hajaonekana huko kijijini, na wao walijua labda amekubali kusibiri huko hospitali …! Taarifa hiyo ikawaacha mdomo wazi na  kuwaacha kwenye mashaka kuwa huyo mama kaenda wapi!
‘Au kagundua kuwa sio yeye na mtoto sio wa kwake, na kaamua kuishia!..mimi bado nina mashaka nay eye…?’ akasema nesi
‘Lakini dalili na vielelezo vyote kama alivyotupa docta kijana vinaendana na yeye, sasa sidhani kama hoja ikawa sawa, labda…kama yupo mama mwingine mwenye sura kama hiyo…labda, …mimi naona tungoje, kama ndio yeye lazima atarudi tu, kama sio yeye basi tutakuwa na kazi ya ziada, ya kumtafuta mama halali wa mtoto, vinginevyo, inabidi uwaombe ndugu zako waendelee kumkubali huyo mtoto kama mtoto wao..’ akasema docta bosi wa nesi.
‘Hilo la ndugu zangu kumchukua huyu mtoto kama wao, sidhani kama litawezekana kwasababu shemeji yangu anasema akimwangali huyo mtoto anamkumbuka mbaya wake, kasababau wanafanana sana..’ akasema nesi.
‘Sasa ina maana shemeji yako anamjua baba wa mtoto, hawezi kuwasiliana naye..?’akauliza docta
‘Una maana chui awasiliane na mbuzi …inawezekana kweli…’ akaseme nesi kwa utani na wote wakaishia  kucheka. Na moyoni mwa nesi akawa anavutika na hisia zake za kumkumbuka docta kijana, na pia akimuwaza huyo docta kama angelikuwa mume wake ingekuwa ni furaha sana, …lakini docta huyo ni mume wa mtu…akajisemea moyoni kuwa docta kijana ndiye mume mtarajiwa…sijui kwa vipi!
Mazungumzo ya docta na nesi kwenye simu yaliishia bila kupata ufumbuzi wa maana, iliyobakia ni kusubiri tu nini kitatokea , kama huyo mama atatokea tena au kuna mama mwingine atakuja kujitambulisha yote kwao itakuwa heri, lakini lazima utaratibu ufuatwe ili, isije ikaleta mgongano baadaye…! Siku ya Jumamosi ikapita, na siku ya Jumapili ikaingia.
Ilikuwa siku ambayo wanafamilia walipnga kukutana  na siku hiyo waliipangia kuwa siku muhimu sana, waliamua kufanya kitafrija kidogo ambacho walikuwa mekipanga awali wakawa wanakiahirisha kwasababu hizi na zile, na hata walifikia kuwa wafanye tafrija hiyo baada ya kujifungua, lakini wakaona siku hiyo ya Jumapili inafaa, kifanyike tu. Waliona pamoja na hilo ni vyema, familia kama familia kukutana na kubadilishana mawazo, wakaitana wanafamilia wote waliopo karibu, na bahati nzuri , wanafamilia wengi walikuja , na ikaandaliwa tafrija fupi ya kumshukuru mungu kwa mama aliyekuwa hakutarajiwa kupata mtoto , sasa ni mja mzito, na mambo mengine ya kifamilia, na nesi akajiliza kichwani, hapo ni mimba tu, jei siku akizaliwa huyo mtoto itakuwaje…
Pilika pilika zikaanza, watu na majirani wakajumuika na wahusika wakaitambulisha ile tafrija fupi kuwa ina maana gani.
Wakati watu wamejimwaga na vyakula vinaliwa, hakuna aliyekuwa na wazo lolote zaidi ya ile sherehe, dada wa nesi na nesi walikuwa wamevalia sare, na mume mtu alikuwa kavalia suri yake safi wakawa wamekaa pale mbele kama wahusika wakuu, picha za kumbukumbu zikapigwa.
‘Mwiteni mtoto wetu  naye apate picha ya kumbukumbu…’ akasema dada wa nesi, akiwa na mama yule mtoto wa kufikia na hata nesi akasema hivyo. Hoja hii aliipinga shemeji mtu, akaondoka pale walipokuwa wamekaa na kuitenga,  kwani tangu mtoto yule achwe hapo, amekuwa hana raha kabisa. Na alikuwa mbalimbali na huyo mtoto, na ikitokea bahati wakakutana , yeye humkwepa, licha ya kuwa mtoto kila mara alikuwa akimlilia na kumuita `baba, baba…’
Kuna mara nyingine aliingiwa na huruma na kumchukua , na akimtizama usoni ,…anakuwa kama anakumbuka kitu, basi humwachia …na hutafuta mwanya wa kutoka hapo nyumbani , na kwenda zake nje kukutana na marafiki zake. Mkewe alimshauri sana kuwa anachofanya siyo jambo la kiungwana, kwani yule mtoto hana kosa kabisa, ni kimumbe ambaye hajui kabisa nini kilitokea…mumewe anamjibu kuwa yeye hajui machungu gani aliyoyapitia , na mtoto huyo humtonesha donda ambalo lilishaanza kupona! Na mazungumzo hayo hayaishii vyema, mume mtu anaamua kuodnoka, ili wasiendelee kubishana
‘Mtoto haonekani…’ akasema dada mmoja ambaye ni ndugu kwa kupitia kwa babu  yao,  yaani baba yake nesi na baba wa huyo dada wanazaliwa tumbo moja kwahiyo kiutaratibi huyo dada anamwita nesi au dada yake nesi `dada ’ wao wanaishi kijijini ambapo familia yao ndipo ilipoanzia na alikuja hapo toka huko kijiji kingine kwa ajili ya kuishi na ndugu zao hawo kwa vile dada yao ni mja mzito basi aliletwa kuja kusaidia kazi mbalimbali.
‘Umemwangalia huko alikokuwa akicheza na wenzake..’ akauliza nesi
‘Kote nimeangalia na nimewauliza wenzake wanasema hawajui wapi ameenda, wengine wanasema aliondoka kuwa anakuja ndani kunywa maji lakini hakurudi tena,, wengine wanasema alikuwa akiangalia ngomea iliyokuwa ikipita , na huenda ameongozana nayo…’ ilimradi kila mtoto alisema lake. Ikawa shughuli kumtafuta mtoto kaenda wapi. Mpaka inafika usiku haijulikani wapi mtoto kaelekea.
‘Sasa tutafanyaje maana hii sasa ni kesi akija mama wa mtoto tutamwambia nini…’ akaanza kulalamika nesi
‘Bwanae, naona unataka kutuharibia tafrija yetu, niliwaambia huyo sio daamu yetu atatuletea mabalaa hamtaki kusikia, anagalieni tangu aletewe hapa, kila mara linazuka jambo la utata..mnaona sasa, …mimi simo kwa hili na wala msinishirikishe, maana huyo mwanamke balaa akija hapa atanizukia mimi na kuniletea mambo nisiyo yataka…’ akasema shemeji mtu.
‘Hili ni letu sote kwasababu mtoto huyu aliachwa hapa kwenye nyumba yako, huwezi kulikwepa cha muhimu ni kusaidiana jinsi ya kumtafuta , na bora tuwape taarifa polisi…’ akasema mke mtu.
‘Nani aende polisi, yaani nipoteze muda wangu kwa ajili ya….’ Aksema mume mtu na kabla hajamaliza simu ikaiita, na nesi alipoitizama simu yake akakuta anayeiita ni docta, akasogea pembeni huku akiwa na wasiwasi atamwambiaje huyo docta bosi wake ambaye alishachukua dhamana ya usalama wa huyo mtoto!

Jamani sio kwamba napenda kuandika kiduchu, bali ni majukumu, na sipendi siku ipite bila kuwakilisha angalau kidogo, na hi ni sehemu amabayo ilibakia nyuma, kwani mhadithiaji  alikuwa mama wa jamaa anayetupa hiki kisa na huyu mama alikuwa kapekwa India, …tuendelee kuwepo ili tukamilishe hiki kisa na kama kuna sehemu nimeruka naomba mnihabarishe, ili tumalizie vyema! Karibu sana, na kumbukeni maoni yenu ndiyo yatakayofanya kisa hiki kiwe na mwisho wenye mvuto zaidi!

No comments: